12 Jan 2016

MKONO WA MWANDISHI. Na. Kamanda Amata

Katika program yetu hii ya Mkono wa Mwandishi, tutaangazia kazi mbalimbali za riwaya kutoka kwa waandishi tofauti wachanga na wakongwe.

Hapa tutapitia riwaya, tamthiliya na hadithi fupi na kuangalia dhima nzima ya mwandishi iliyojificha nyuma yake; sababu za kuandika, nani alimlenga na nini kilimsukuma. Najua wengi wetu ni wapenzi wa riwaya lakini ni vigumua ujua mwandishi kwa nini ameandika kazi hiyo. Swali hili ‘kwa nini?’ wengi tunajiuliza mara nyingi; kwa nini huyu mwandishi kaandika kazi hii? Alifikiria nini? Hapa katika kurasa hii utajua kila kitu juu kazi ya mwandishi Fulani na kama utakuwa hujaisoma kazi hiyo basi utapata ‘link’ ya kuiweza kuisoma mara moja baada ya kumaliza kupitia program hii.

Kwa nini tumeiita ‘Mkono wa Mwandishi’?

Daima mwandishi hutumia mkono wake kuweza kuandaa kazi yake, awe anatumia kompyuta au kalamu bado mkono wake ni kiungo chake muhimu sana katika kazi yake. Kwa hiyo ‘Mkono wa Mwandishi’ ndiyo hasa uliyoifanikisha kazi hiyo kuja kwako, kukupoa burudani, ukaburudika, ukafurahi, ukahuzunuka, ukatoa machozi, ukatukana, ukashangilia, ukaudhika. Yote haya yako nyuma ya mkono wa mwandishi.
Richard Mwambe atakuwa pamoja nawe katika program hii akiuangalia mkono wa kila mwandishi katika kazi hii tukufu ya riwaya.

MKONO WA MWANDISHI – awamu ya 1.

Leo katika Mkono wa Mwandishi tunauangalia mkono wa Richard Mwambe katika kazi yake ya HAMUNAPTRA. Hii ni kazi ambayo iliwahi kutikisa akili za wasomaji, ikawachanganya na kuwaacha midomo wazi kuanzia jina la riwaya hiyo mpaka umbo lenyewe la kazi hiyo.
Kazi hiyo ambayo mwandishi anatupeleka katika miji ya Hamunaptra, Giza, Jamunah, India na sehemu zingine ambazo hazishikiki wala kugusika kibinadamu pia anatukutanisha na Seidon kama mhusika mkuu msaidizi akimsaidia Amatagaimba katika kazi ngumu ya kurudisha fuvu la kiumbe wa kale Cleopas.
Wengi walihoji Hamunaptra nini?
Hamunaptra ni mji, mji wa kufikirika, mji wa wafu ambao upo chini ya ardhi kadiri ya mkono wa mwandishi jinsi ulivyotueleza. Katika aya ya kwanza kuueleza mji huo na jinsi ya kuufikia, mwandishi anaturudisha mpaka mwaka 1850 katika nchi ya India ambako Wakoloni wa Kiingereza walikuwa wakiwatumikisha wenyeji katika kujenga reli… hebu soma kidogo kipande hiki :-
>>>>>>>>>>>>>>>
1850
Sehemu Fulani huko India

Jua liliwaka kwelikweli, vibarua walifanya kazi ngumu ya kuvunja mawe na kusogeza hapa na pale, kukusanya vyuma ili kutandika reli mpya kwa manufaa ya koloni la Uingereza. Askari wa Kiingereza walisimama kando wakipuliza moshi wa kiko na cigar, huku mijeledi ikiwa viunoni mwao, hutakiwi kusema umechoka wala unaumwa, utafanya kazi mpaka pumzi yako iishe.
Haikuwa rahisi hata kidogo, mataruma mazito yalivutiwa hapo na kazi ya kuunganisha njia ya reli iliendelea chini ya engineer wa kiingereza aliyejawa na dharau na nyodo kupita kiasi.
Ili kupata mawe yanayotakiwa hasa katika kazi hiyo iliwabidi kupasua majabali makubwa na miamba ya kutisha, vibarua wengi walipoteza maisha kwa kupigwa na mawe hayo yaliyoruka huku na huko. Baada ya kupasua mawe hayo an kuyamaliza sasa walianza kuchimba kuelekea chini. Hakukuwa na mashine kama hizi tulizo nazo wao walichimba kwa dhana duni lakini zilikuwa bora kwa wakati huo.

Prakesh Minto, kibarua aliyeipenda kazi yake aliinua juu sururu yake na kuitelemsha ili kupiga jiwe lililoonekana kujitokeza katika shimo hilo, kabla sururu ile haijatua alijikuta ikimtoka mikononi na kuruka pembeni, kisha alisikia sauti zikiongea maneno yasiyoeleweka. Prakesh alichanganyikiwa na kuanza kukimbia hovyo. Waingereza wale waliokuwa hapo katika kusimamaia shughuli ile walimuona Prakesh kama aliyeruykwa na akili, walimpiga risasi na kumuua. Kisha wakasogea eneo lile, kijana mwingine alikuwa akichimba lufuata kitu kama ukuta. Walipoona ukuta ule hauna dalili ya kufika mwisho ndipo walipoomba wataalamu kutoka Uingereza kuja kutoa msaada katika hili.

Baada ya Miezi kadhaa ya kuchimba na kusafisha eneo lile walijikuta mbele ya mji mkubwa, mji wa kale ambao kwa wakati huo ulikuwa umesha zama ardhini kwa karne na karne, hata waenyeji walikuwa wakiishi hapo miaka hiyo hawakulijua hilo. Kuta zenye nguvu, nguzo kubwa, milango iliyotengenezwa kwa mbao ngumu ambazo zilidumu hapo bila kuliwa na nondo.
Paul Smith, aliivua kofia yake aina ya pama na mkono mmoja alikuwa kajishika kiuno. Mtaalam huyo wa mambo ya kale, alijivunia sana ugunduzi wake, aliendelea kupiga mluzi akiimba moja ya nyimbo za kwao. Baada ya kuhakikisha kuwa eneo lote liko safi, waliadhimia sasa kuingia ndani ya mji huu kujionea kilichopo, mioyoni mwao waliamini kuwa sasa utajiri upo jirani. Walijaribu kuvunja mlango lakini hata hawajathubutu mlango ulifunguka wenyewe na kiza kinene kiliwa karibisha.
>>>>>>>>>
Hapa hatujaelezwa kinagaubaga jina la mji huo lakini utagundua kuwa huu ni mji uliokuwapo ila ukafunikwa na tufani za mchanga wa jangwani, mkono wa mwandishi unaendelea kutuainishia katika jina la kazi hiyo kuwa ni ‘Mji uliopotea’.
Mkono huu wa mwandishi unaendelea kutembea na kutuonesha ugumu wa safari hiyo ya hatari iliyowakutanisha Seidon na Amatagaimba, kati yao tunaoneshwa utaofauti wa fikra; Seidon alitumwa na babu yake kwenda kuchukua fuvu hilo ambalo lilifichwa huko mapangoni na kuwekewa ulinzi madhubuti wa mwindaji mashuhuri wa Misri, Orion ambaye inasemekana shabaha yake haina makosa.
Katika kunogesha kisa hiki mwandishi anatuambia kuwa Seidon alikaidi moja ya masharti aliyopewa na babu yake….. soma kipande hiki :-
>>>>>>>>>>

“Sogea hapa Seidon,” babu yake alimwita Seidon na kuichukua mikono yake na kuipachika mapajani kama ishara ya kula kiapo.
“lazima uwe muaminifu, babu wa babu zako Vernad alifanikiwa kulipata fuvu hilo kutoka katika mikono ya Wamisri baada ya kupambana kiume na shujaa Orion, na sasa lipo katika mikono ya Waajemi baada ya kuja na kutunyang’anya apa hapa kwetu, ukiwa njiani usitamani mwanamke wala kulala nae, la, utapata nuksi ambayo kazi niliyokupa itakushinda” Babu yake alimaliza wosia na seidon akatoka na kuketi chini.
“Babu nitahakikisha nafanikisha hilo kwa uaminifu.” Alijibu kwa utii.
“Chukua upanga wa Vernad hapo juu, na roho yake ikuangazie katika mapito yako.”

>>>>>>>>>>
Seidon anafika Jamunah na kukutana mwanamke mlaghai mwenye umbo na uzuri wa ajabu na utamu wa kila namna, anajisahau na kuvunja mwiko aliyowekewa na babu yake.
Baada ya kufanya hilo nini kinamtokea…….?
Endelea kufuatana na Mkono wa Mwandishi katika kazi yake hii ndani ya kurasa ya JAMVI LA SIMULIZI ZA KUSISIMUA.

Kazi ya uandishi hasa wa riwaya kama ilivyo kazi nyingine ngumu, naweza kukwambia ni ngumu kwelikweli kuliko unavyofikiria. Ndugu msomaji hebu ifikirie sanaa hii ambayo mwandishi anatengeneza maneno zaidi ya 20000 kutoka katika maneno yasiyozidi matano. Anakujengea kisa na kukiweka ndani ya akili yako na kukubadili katika hali ambayo wewe mwenyewe haujaifahamu labda mtu wa pili.
Ndani ya kazi hii tutanapata kujifunza mambo mbalimbali licha ya burudani, mkono wa mwandishi hautaki tu kukuburudisha bali kukufundisha wewe msomaji na kukueleimisha.
Amatagaimba, nyota wa riwaya hii ya adventure, anamwongoza vema Seidon katika safari yake hiyo baada ya kumwambia ukweli kuwa anakosea yeye na watu wake, soma kipande hiki:-
>>>>>>>>

“Vizuri sana, na wote hamjui, wote kabisa hamjui siri ya fuvu la Cleopas, sasa sikiliza, Cleopas na wenzake sita ndio walikuwa wakiiendesha dunia ya chini, dunia ya wafu, dunia ya waliolala, wao daima wamejipanga kwa mtindo huu, kushoto wapo watatu Aminus, Petrius na Segidus na kulia wapo watatu Sagitarius, Hesmepitus na Sectogamus, Cleopas yupo mbele katikati yao, ukiwaweka wote hivo ndio ule mkao wao unaitwa Klakos sasa waingereza miaka ile waling’oa fuvu la Cleopas ndiyo wakaleta ukame duniani maana chemchem, mito, mimea vyote si vinaota kutoka chini ni baraka za Klakos. Laana aliowapa ndio ile vita ya dunia huko Ulaya na matatizo mengine” Amata alimwangalia Seidon ambaye alionekana kukodoa macho tu.
“Umenielewa?” alimuuliza Seidon ambaye alibaki midomo wazi, “Sasa unatakiwa uchukue lile fuvu ulirudishe kule kwa Cleopas kwenye mji uliopotea, mji wa wafu, Hamunaptra, mji ulio chini ardhini”.
>>>>>>>>>
Baada ya hapo Amatagaimba na Seidon wanaunganisha nguvu na kupambana na nguvu za Mashariki kutoka kwa Malkia wa majini ya kike wan chi ya Soria Sherhazad ambaye alimlaghai Seido katika safari yake ya kwanza.

*********

Katika upande wa pili wa hadithi hii tunaona Mkono huu wa mwandishi unaturudisha sasa, katika ulimwengu wa sasa katika Chuo kikuu cha Dar Es Salaam. Hapa anatuonesha wanafunzi wa kitivo cha mambo ya kale wakijiandaa kwenda katika safari ya mafunzo na wanachagua kwenda Misri kuona Mapiramidi.
Mkono wa Mwandishi unatuletea kwa upya kazi hii ambapo msomaji anapata kuchanganyikiwa na kutakiwa kuituliza akili yake kuelewa kisa hiki kilichoandikwa kwa umahiri kwa mtindo wa kurudi rudi nyuma ‘Kisengere nyuma au flashback’.
Kati ya wanafunzi hawa kuna mmoja wao anayejikuta anaandamwa na mauzauza ndani ya mapiramidi hayo, mwisho ajali mbaya inatokea ndani yake, mwanafunzi mmoja anapoteza maisha na mwingine Anna Davis anaangukia kwenye shimo kubwa sana na kupoteza fahamu.

Kiukweli kabisa mwandishi wa kazi hii anakuonjesha maisha ya ulimwengu wa chini, visa na mikasa vilivyopangwa kisanaa kabisa vitakufanya upumue kwa nguvu kwa jinsi alivyotumia vyema mkono na kalamu yake.
Katika aya ya mwisho kabisa ya riwaya hii ndipo mwandishi anapokutaka utabasamu na kusema neno lolote la kuitukuza kazi yake. Na hii yote ni kazi ya Mkono wa Mwandishi.
Itafute sasa kazi hii na uone jinsi Mkono huu ulivyotembea na kucheza na akili yako vyema.
Asante!

:::Makala hii imeandaliwa na Richard Mwambe. Wiki ijayo tutaangazi Mkono mwingine wa mwandishi, usikose saa kama hii, hapa hapa.
0766974865.


Ukitaka kuisoma riwaya hii iliyoangazwa leo bofya link hii....https://web.facebook.com/JamviLaSimuliziZaKusisimua/?fref=ts
MKONO WA MWANDISHI

Translate